MKOA wa Morogoro umeteuliwa na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) mwaka huu kufanyika maadhimisho ya Ijumaa Kuu na Sikukuu ya Pasaka Kitaifa.
Ibada ya kesho ya Ijumaa Kuu itafanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Patrick, Jimbo Katoliki la Morogoro na itaongozwa na Askofu wa jimbo hilo, Askofu Telesphor Mkude.
Aidha, Ibada ya Pasaka itafanyika katika Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Morogoro na itaongozwa na Askofu Godfrey Sehaba.
Katibu Mkuu wa CCT, Dk Leonald Mtaita amesema kuwa ibada zote mbili zitafanyika mkoani Morogoro na ya kesho inatarajiwa kuanza saa tisa alasiri, wakati ya Pasaka itafanyika asubuhi kama kawaida.
Akizungumzia ujumbe wa Pasaka kwa Mwaka huu, Dk Mtaita alisema, “Kila Kanisa litakuwa na ujumbe wake, lakini msisitizo wa pamoja kwa CCT ni kuhamasisha amani kwa jamii na bidii ya kufanya kazi halali ili kupata kipato”
Dk Mtaita aliongeza kwa kusema kuwa; “Tunawatakia heri za sikukuu hizi na Pasaka mwaka huu iwe ya mabadiliko kuanzia ngazi za familia hadi jamii nzima, waumini wanapaswa kufanya kazi kwa bidii na viongozi wao tunawahakishia kuwa yapo matumaini makubwa ya kufanikiwa kimwili na kiroho.”
Ibada ya Ijumaa Kuu hufanyika kote duniani na waumini wa dini ya Kikristo kukumbuka kifo cha Mwokozi Yesu Kristo na Pasaka huadhimishwa ikiwa ni kumbukumbu ya Kufufuka kwa Yesu.
Mwaka jana, maadhimisho ya Ibada hizo kitaifa yalifanyika Dar es Salaam ambapo Ijumaa Kuu Ibada ilifanyika katika Kanisa la Columbas Presbyterian na Pasaka katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph.