Askofu Mokiwa alisema kuwa, Wakristo wa visiwani Zanzibar wanaishi kwa hofu ya kutishiwa maisha kwa kupigwa mawe na wanaonekana kama daraja la pili, lakini Serikali haichukui hatua madhubuti. “Matukio yote hayo yameripotiwa polisi, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa. Tumesikia mkisema (Serikali) eti wanaofanya hivyo ni wahuni. Sisi tunasema hiyo ni lugha ya kututia ganzi. Wale siyo wahuni ni wahalifu na kuna taratibu za kuwachukulia hatua za kisheria. Serikali inakemea lakini haina ‘confidence’ (haijiamini),” alisema Askofu Mokiwa.
Aliitaka pia Serikali kueleza mikakati inayochukua na kuwataja majina wahalifu waliokamatwa ili waamini kama kweli hatua zimechukuliwa. Alisema Serikali pia inapaswa kuchukua hatua kwa vikundi vya dini vinavyohubiri siasa kinyume na masharti waliopewa. “Siyo dhambi watu kutaka nchi yao au Serikali yao, lakini masuala haya (ya kuchomewa makanisa) hayana uhusiano wowote na Muungano). Basi kuwe na majadiliano na vikundi hivi ili kuleta maridhiano.
Akijibu malalamiko hayo, Waziri Aboud alisema atayafikisha yote kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Shein na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete bila kupunguza hata nukta. Alikiri Serikali kuzembea katika matukio hayo, lakini akasisitiza umuhimu wa viongozi wa dini kutoeneza lugha za chuki. “Lazima tuwe na mkakati wa pamoja na kuhakikisha tunapambana na wote wanaoeneza chuki. Uvumilivu wenu mliouonyesha ni mkubwa hivyo tunaomba muendelee. Hao wanaofanya hayo tutahakikisha tunawafikisha kwenye vyombo vya sheria.” Alisema Waziri Aboud.
Akizungumzia uhusiano kati ya Wakristo na Waislamu visiwani humo, Waziri Aboud alisema tangu kanisa la kwanza lilipoanzishwa visiwani humo mwaka 1870, wamekuwa wakiishi kwa kushirikiana bila kubaguana hadi siku za hivi karibuni.
Alipoulizwa waandishi wa Habari kuhusu ukimya wa Rais Shein tangu machafuko hayo yatokee, Waziri Aboud alihamaki akisema ameshatoa matamko mengi kwa nyakati tofauti. “Rais ameshazungumza kwa nyakati tofauti, akiwa hapa na huko Pemba… Ameshazungumza sana, lakini ninyi hamwandiki tu. Hata sasa amenituma nizungumze, sisi ndiyo tunaomwakilisha. Lakini ameshazungumza mno.”
Uamsho yakana Mmoja wa viongozi wa Jumuiya ya Mihadhara ya Kiislamu (Uamsho), Sheikh Farid Hadi Ahmed amesema hawahusiki na vitendo vya kuchoma na kuharibu makanisa na kuwalaani watu wanaounganisha kundi hilo na tuhuma hizo. Akizungumza katika Msikiti wa Mbuyuni uliopo eneo la Darajani mjini hapa, Sheikh Ahmed alisema kuwa kundi hilo linafuata taratibu katika harakati zake hivyo halipaswi kulaumiwa kwa vurugu. “Lakini tuna wasiwasi na hawa wanaolipua makanisa na sisi tunawalaani vibaya, hawa tunaamini ndiyo walewale waliokuwa wakisimama na kutukana matusi, tena wana visu, wana nondo, wana pesa…” alisema Sheikh Ahmed.
CHANZO: Gazeti la Mwananchi