Na Mwl. Christopher Mwakasege
Biblia inatuambia kwamba Mungu huyu ambaye amesema anafuta na kuyasahau makosa yetu, kwa ajili yake mwenyewe, anakaa ndani ya watu wote waliompokea. Hebu soma na kutafakari maneno yafuatayo:
“Hapa mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Naye Neno akafanyika mwili, akakaa kwetu, nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli. Wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake, waliozaliwa,si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu” (Yohana 1:1, 14, 12, 13).
Yesu Kristo anapoingia ndani ya moyo wako, baada ya wewe kumwamini na kumpokea, unapewa uzima wa milele ndani yako, na unaanza maisha mapya.Imeandikwa kwamba, ” Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! Yamekuwa mapya.”(2Wakorintho 5:17)
Utu mpya unazaliwa ndani yako, maisha, mawazo, matendo, maneno, yanatakiwa kubadilika Yesu Kristo aingiapo ndani yako. Pia, kusamehe kwako kunabadilika kunakuwa kupya.Lakini utaona kwamba watu wengi waliozaliwa mara ya pili, na kumkiri Kristo kuwa ni Bwana na Mwokozi wao, bado wanaendelea kusamehe kama zamani. Biblia inasema ” ya kale yamepita, tazama!yamekuwa mapya” (2Wakorintho 5:17).
Kwa maneno mengine ni kwamba kusamehe kwako ulivyokuwa unafanya zamani, hakuhitajiki tena, tazama! Kusamehe sasa ni kupya. Tabia ni mpya.Zamani ulisamehe lakini bado ulikumbuka makosa uliyofanyiwa. Tena ulisamehe si kwa ajili yako bali kwa ajili yake aliyekukosea na wakati mwingine ulitaka uthibitisho kwanza kuwa kosa hilo halitarudiwa na ndipo usamehe. Ni lugha ya kawaida kusikia mtu akisema ‘nasamehe lakini sitasahau’.
Katika maisha mapya utatakiwa usamehe na kusahau kwa ajili yako mwenyewe, ili kuomba kwako kusizuiliwe na baraka zako zisizuiliwe. Kwa kuwa imeandikwa hivi: “Yeye asemaye yakuwa anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe vile vile kama yeye alivyoenenda” (1Yohana 2:6)
Wewe unayesema kwamba una Kristo ndani yako, basi inakupasa kuenenda kama Kristo alivyoenenda alipokuwa hapa duniani katika mwili.Kwa kuwa Kristo alisamehe na kusahau, basi na wewe inakubidi kusamehe na kusahau.
Hatua tano zifuatazo zitakupa msingi imara wa kuishi siku zote katika upendo na amani na jirani zako na ndugu zako. Na pia, zitafungua milango mipya ya uhusiano wako na Mungu utakaoinua huduma yako katika kumtumikia Mungu. Na zaidi ya yote zitakuweka huru na magonjwa mengi yanayokusumbua:
1. FAHAMU KUWA SI WEWE BALI KRISTO.
“Nimesulibiwa pamoja na Kristo, lakini ni hai, wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu ambaye alinipenda akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu” (Wagalatia 2:20)
“basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu, yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi.Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu” (Wakolosai 3:1-3)
Mistari hii michache ni baadhi tu ya ile inayotufunulia mambo yaliyofanyika ndani yetu tulipompokea Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wetu.Si wewe unayeishi, bali ni Kristo aliye ndani yako. Na uhai ulio nao sasa, baada ya kuzaliwa mara ya pili, unao katika imani ya Mwana wa Mungu.Soma tena mstari huu: “….. Kwa maana mlikufa na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu.”
“Kwa maana mlikufa.” Utu wako wa kale, na mtu wa kale ndani yako alikufa siku ulipompokea Kristo maishani mwako. Kilichofuata ni uzima wa Kristo, katika utu mpya ukidhihirishwa katika maisha yako.Sasa unaweza kuelewa kwa nini Yesu Kristo alisema awachukiae ninyi, amenichukia mimi. ” ( Yohana 15 :18)
Mtu akikufanyia ubaya, usione kuwa anakufanyia wewe, ona kama vile Mungu aonavyo kuwa, ubaya huo anafanyiwa Kristo aliye ndani yako.Mtu akikutukana, akikusemea mabaya, akikupiga, fahamu kuwa si wewe anayekufanyia hayo, bali Kristo aliye ndani yako!Kuthibitisha haya Biblia inasema: “Vita hivyo si vyako ni vya Bwana” (2 Mambo ya Nyakati 20:15). Ukiwa na wazo hilo katika roho yako, chukua hatua ya pili ifuatayo:
2. MPENDE ADUI YAKO UMUOMBEE.
“Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako na umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi ….” (Mathayo 5:43, 44)
Jambo ambalo liko wazi ni kwamba hakuna msamaha wa kweli pasipo upendo, “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtuma Mwanae …” (Yohana 3:16). Kilichomfanya Baba Mungu kumtuma Yesu Kristo duniani ni Upendo. Alitupenda sisi mno, alitupenda upeo wakati bado tulipokuwa tungali wenye dhambi. Na kuudhihirisha upendo huo, Yesu Kristo alizaliwa duniani na kufa masalabani ili sisi tupone.
Msamaha wa kweli unadhihirisha upendo ulio ndani ya mtu. Pasipokuwa na upendo, kusameheana hakupo. Palipo na upendo wa kinafiki, pia pana kusameheana kinafiki. Kusameheana hakuonekani siku hizi, katika ndoa, kati ya ndugu, kati ya majirani, kati ya watu wa Mungu, KWA SABABU UPENDO WA WENGI UMEKWISHA POA!
Watu siku hizi wanafanya kile ambacho Yesu Kristo aliwaambia wasifanye. Yesu alisema, ” Wapendeni adui zenu.” Lakini, unaona katika watu wa Mungu, chuki imejaa, ndoa zinaharibika kwa sababu ya chuki, undugu unakufa kwa sababu ya chuki. Na ni hao wanaosema kuwa wameokoka na Yesu Kristo yumo ndani yao. Usiwachukie wanaokuudhi, wapende.”
Yesu Kristo anakuambia watu wa dunia wanawapenda wanaowapenda na kuwachukia wanaowachukia, lakini wewe si wa dunia hii, wapende hata wale wanaokuchukia na ili kuonyesha kuwa unawapenda kweli, uwaombee! Kwa nini Yesu Kristo, alisema “Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi?”
Ni, “Ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi, mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je? Nao hawafanyi kama hayo?” (Mathayo 5:45- 47).
Ulipompokea Kristo, ulipokea upendo mpya ndani yako, unaokuwezesha kufanya mambo ambayo mtu wa kale aliyekuwa ndani yako asingeweza kufanya. Mtu mpya ndani yako ana upendo mpya. Upendo huu mpya, una tabia mpya, na mambo mapya.
“Upendo huvumilia, hufadhili, upendo hauhusudu; upendo hautakabari; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli huvumilia yote; huamini yote; hustahimili yote. Upendo haupungui neno wakati wo wote” (1Wakorintho 13:4 – 8).
Upendo huu umo ndani yako, na ndio unaokufanya uwe kiumbe kipya. Ni upendo ulio hai (Warumi 5:5). Ni upendo unamuondolea mtu chuki, uchoyo na ubinafsi. Kwa upendo huu, Bwana Yesu anataka uwapende adui zako, na kuwaombea pia ili wasamehewe na Mungu juu ya makosa waliyoyafanya.
Kwa upendo huu fanya yale ambayo ulikuwa huyafanyi zamani. Kama ulikuwa husalimiani na adui yako, chukua hatua ya upendo, msalimie na ikibidi mtembelee nyumbani mwake. Kula pamoja naye, furahi pamoja naye, na omba pamoja naye.
Kuna watu wengine hawasalimiani wala kutembeleana na wazazi wao, au baba au mama, kwa sababu ya mambo yaliyofanyika zamani ambayo hawakuyapenda.
Sasa, chukua hatua waandikie barua, na uwatembelee kwa maana upendo wa Kristo umekuweka huru, na chuki na kinyongo. Kumbuka unayafanya hayo kwa ajili yako mwenyewe ili maombi yako yakubaliwe mbele za Mungu.
Nafahamu kwa jinsi ya mwili, na kwa kutumia akili ya kibinadamu hatua hizo ni ngumu kuchukua. Ni kweli, lakini kumbuka si wewe unayeishi, bali Kristo ndani yako. Na unayaweza yote (pamoja na kuwapenda adui zako) katika yeye akutiaye nguvu (Wafilipi 4:13)
Upendo unavunja nguvu za uadui. Usimuone jirani au ndugu ni adui tena. Kama vile wewe ulivyo kiumbe kipya ndani ya Kristo, kwa jicho la upya huo waone adui zako kuwa ni rafiki. Anza uhusiano mpya nao.
“Lakini nawaambia ninyi mnaosikia wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi” (Luka 6:27,28)
SOMO HILI LITAENDELEA JUMAPILI HII JUNE 24, ENDELEA KUTUTEMBELEA.
Watumie rafiki zako kupitia;